Tanzania na Afrika Kusini zaahidi kuimarisha ushirikiano wa pande mbili
2023-03-17 22:01:29| cri

Viongozi wa Tanzania na Afrika Kusini wameahidi kuimarisha ushirikiano wa pande mbili kati ya nchi hizo.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa jana alhamis mwishoni mwa ziara ya siku mbili ya rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan nchini Afrika Kusini imesema, rais Samia na mwenzake wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa wameahidi kuimarisha urafiki na mshikamano uliopo kati ya nchi hizo mbili, na kuahidi kuendelea kujenga uhusiano huo kwa ajili ya manufaa ya watu wa nchi hizo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, viongozi hao wameonyesha nia ya kuboresha na kupanua ushirikiano na uratibu katika sekta mbalimbali ikiwemo ulinzi na usalama, biashara na uwekezaji, kilimo, mazingira, sayansi na teknolojia na maendeleo ya miundombinu.

Viongozi hao pia walibadilishana maoni kuhusu masuala mbalimbali ya kikanda, ya bara la Afrika na ya kimataifa yanayofuatiliwa na pande hizo mbili.