UM: Uchumi wa Afrika watarajiwa kukua kwa asilimia 3.9 mwaka huu
2023-03-17 09:02:59| CRI

Kamati ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA), imesema uchumi wa Afrika kwa mwaka huu unatarajiwa kukua kwa asilimia 3.9, ikilinganishwa na asilimia 3.6 za mwaka jana.

Akiwasilisha ripoti kuhusu maendeleo ya kiuchumi na kijamii barani Afrika kwenye kikao cha 55 cha kamati hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Uchumi na Utawala Bora wa UNECA Bw. Adam Elhiraika, amesema ukuaji wa pato la jumla la bara la Afrika ulipungua kutoka asilimia 4.6 za mwaka 2021 hadi asilimia 3.6 mwaka 2022, lakini ukuaji huo unatarajiwa kurudi hadi asilimia 3.9 kwa mwaka huu.

Kudorora kwa uchumi wa dunia, kupanda kwa bei kunakochochewa na mgogoro wa Ukraine, mabadiliko ya tabia nchi na kuzorota kwa hali ya kimataifa ya kiuchumi na kifedha kumeathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa Afrika kwa mwaka jana.

Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, Afrika ndio eneo lenye ongezeko la kasi zaidi baada ya eneo la Asia Mashariki na Kusini.