Kuhusu madeni ya Afrika, kurudia uongo hakubadilishi ukweli
2023-03-20 10:02:42| CRI

Shirika la Fedha la Kimataifa, Benki ya Dunia, na nchi mwenyekiti wa zamu wa G20 hivi karibuni zilifanya mkutano wa kimataifa kuhusu masuala ya madeni. Baadhi ya wanasiasa na vyombo vya habari vya Marekani na nchi Magharibi wamechukua fursa hiyo kuipaka matope China kuhusu madeni yake kwa nchi za Afrika, na kudai kuwa China imeweka “mtego wa madeni” barani Afrika. Lakini ni wazi kuwa, hata uongo ukirudiwa mara ngapi, ukweli lazima utathibitika.

Kutokana na kuendelezwa kwa mifumo ya ushirikiano ikiwemo Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) na pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” (BRI), uhusiano wa kirafiki kati ya China na Afrika umepata maendeleo makubwa katika nyanja mbalimbali, na Afrika pia imekuwa moja ya sehemu zinazovutia uwekezaji zaidi wa China. Lakini Marekani na nchi nyingine za Magharibi hazipendi kuona hali hiyo, na wamenyooshea kidole uhusiano kati ya China na Afrika mara kwa mara, na kubuni uongo kuhusu madeni na uwekezaji wa China barani Afrika.

Kauli ya kwanza ambayo si ya kweli ni kwamba, China inatafuta maslahi ya kisiasa kupitia uwekezaji na mikopo barani Afrika. Ukweli ni kwamba nchi za Afrika zinahitaji msaada wa haraka wa kifedha kutoka nje kwa ajili ya maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii. Tangu mwanzoni mwa karne ya 21, China imeunga mkono maendeleo ya uchumi wa Afrika na kuipatia Afrika njia mpya za kupata madeni, ambayo ni tofauti na “Klabu ya Paris”. Wakati wa kufanya uwekezaji na kutoa mikopo kwa nchi za Afrika, China inafuata kanuni za kuheshimu uhuru na mamlaka ya nchi hizo, haiingilii mambo ya ndani yao, na kutoweka masharti yoyote ya kisiasa. Lakini kwa upande wa Marekani na nchi za Magharibi, mara kwa mara, zinaweka masharti ya kisiasa kama vile haki za binadamu na mageuzi ya kisiasa, ili kubadilisha utaratibu wa mambo ya kisiasa ya nchi za Afrika kama zinavyotaka.

Kauli nyingine isiyo kweli ni kwamba, uwekezaji na mikopo ya China vimeleta “mitego ya maendeleo” barani Afrika. Ukweli ni kwamba, China imezingatia zaidi maendeleo ya miundombinu inayohusiana na maendeleo ya uchumi na maisha ya watu inapofanya uwekezaji na kutoa mikopo barani Afrika. Katika zaidi ya miongo miwili iliyopita, China imejenga zaidi ya kilomita 6,000 za reli, kilomita 6,000 za barabara kuu, karibu bandari 20, zaidi ya vituo 80 vya nishati ya umeme, hospitali 130, zaidi ya shule 170, viwanja 45 vya michezo, na zaidi ya miradi 500 ya kilimo katika nchi za Afrika. Ikilinganishwa na China, mikopo iliyotolewa na Marekani na nchi za Magharibi kwa Afrika imetumika zaidi katika nyanja zisizo za uzalishaji, ambapo ni vigumu kuzisaidia nchi za Afrika kupata maendeleo.

Jambo lingine ambalo sio la kweli ni kwamba, madeni mengi ya Afrika yanatoka China, na China inapaswa kubeba jukumu zaidi kwa mgogoro wa madeni barani Afrika. Ukweli ni kwamba, Marekani na nchi za Magharibi zinamiliki mikopo zaidi barani Afrika. Ripoti zilizotolewa na taasisi za kimataifa zinaonyesha kuwa, benki za nchi za Magharibi na wakopeshaji binafsi ndizo zimeleta mzigo mkubwa wa madeni kwa Afrika. Kwa mujibu wa takwimu za Benki ya Dunia, kati ya madeni ya nje ya jumla ya dola bilioni 696 za Kimarekani katika nchi 49 za Afrika, robo tatu zimekopwa kutoka mashirika ya kimataifa ya fedha na mashirika binafsi yasiyo ya China. Ripoti ya utafiti iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Columbia nchini Marekani na Chuo Kikuu cha Oxford nchini Uingereza inaonyesha kuwa, wakopeshaji wa nchi za Magharibi ni chanzo kikuu cha madeni ya nje barani Afrika. Wakati huo huo, ripoti iliyotolewa na Shirika la Misaada la Uingereza “Debt Justice” inaonesha kuwa, asilimia 35 ya madeni ya nje ya nchi za Afrika yanatoka kwa wakopeshaji binafsi wa Magharibi, na kiasi hicho ni karibu mara tatu ya mikopo ya China kwa Afrika, na wastani wa riba ni takriban mara mbili ikilinganishwa na ile inayotolewa na China.

Madai mengine yasiyo ya kweli ni kwamba, China haijabeba majukumu yake yanayostahili kwa juhudi za kurahisisha mzigo wa mikopo barani Afrika. Ukweli ni kwamba, China imejitolea kusaidia nchi zinazoendelea ikiwa ni pamoja na kuzipunguzia nchi za Afrika mizigo ya madeni kwa hatua madhubuti.

Kuanzia mwaka 2013 hadi 2018, China ilifuta jumla ya mikopo 98 isiyo na riba kwa nchi maskini zenye madeni makubwa, nchi zinazoendelea zisizo na bandari na nchi za visiwa vidogo zinazoendelea. Kulingana na ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia, kuanzia mwaka 2008 hadi 2021, China ilifanya marekebisho 71 ya madeni ya nchi zenye pato la chini. China pia imechangia karibu asilimia 45 ya mikopo ilichocheleweshwa kulipwa ya G20.