Kufungua mlango kwa China kuleta fursa zaidi kwa dunia
2023-03-20 10:03:44| CRI

Katika Mikutano Miwili Mikubwa ya China iliyomalizika hivi karibuni, China, kwa mara nyingine, imesisitiza kuwa itahimiza ufunguaji mlango wa hali ya juu. Ikiwa ni nchi ya pili kwa ukubwa wa uchumi duniani, nia thabiti ya kufungua mlango zaidi ya China bila shaka italeta fursa kubwa kwa dunia nzima.

Katika hafla ya kufunga Mkutano wa Bunge la Umma la China, rais Xi Jinping alisema, “Maendeleo ya China yananufaisha dunia, na maendeleo ya China hayawezi kutenganishwa na dunia. Tunapaswa kuhimiza kithabiti ufunguaji mlango wa hali ya juu, kutumia vizuri soko na rasilimali za kimataifa ili kujiendeleza, na wakati huohuo, tunapaswa kuhimiza maendeleo ya pamoja duniani.”. Maneno hayo yamedhihirisha kwa kina mwingiliano kati ya China na nchi nyingine za dunia, na kuonesha nia thabiti ya China ya kuendelea kufungua mlango.

China ni nchi ya pili kwa ukubwa wa uchumi duniani. Maendeleo ya haraka ya China ni injini muhimu ya ukuaji wa uchumi wa dunia. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Benki ya Dunia, kuanzia mwaka 2013 hadi mwaka 2022, wastani wa mchango wa China katika ukuaji wa uchumi wa dunia ulifikia asilimia 38.6, ukizidi jumla ya michango ya Kundi la Nchi 7 (G7). China inayofungua mlango bila shaka itachangia zaidi kufufua uchumi wa dunia.

China ni nchi ya kwanza kwa ukubwa wa biashara duniani. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, thamani ya bidhaa kati ya China na nchi nyingine duniani imeongezeka kwa wastani wa asilimia 8.6 kwa mwaka. China pia imeendelea kufungua mlango katika shughuli za biashara, na kujitahidi kadiri iwezavyo kufikia makubaliano ya biashara huria na nchi nyingine duniani zikiwemo nchi za Afrika. Mwaka 2021, China ilifikia makubaliano ya biashara huria kati yake na Mauritius, ambayo ni makubaliano ya kwanza ya biashara huria kati ya China na nchi za Afrika.  

China ni nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani. Hadi sasa zaidi ya watu milioni 400 kati ya wananchi wake bilioni 1.4 wamekuwa na kipato cha kiwango cha katikati, hali ambayo imeleta soko kubwa kwa bidhaa za nchi nyingine. Parachichi za Kenya, kahawa kutoka Rwanda, matunda ya cheri kutoka Chile, nyama ya ng'ombe kutoka Brazili, zinapatikana kwenye maduka ya China. Kufunguliwa kwa soko la China kumeleta fursa kubwa kwa nchi nyingine duniani.

China pia ni nchi ya kwanza ya kiviwanda duniani. Mnyororo mzima wa viwanda wa China unavutia uwekezaji wa kimataifa. Wakati huo huo, China pia inawekeza nje ya nchi, na kuziletea nchi nyingine haswa zile zinazoendelea uwekezaji pamoja na teknolojia za kiviwanda kupitia majukwaa ya ushirikiano kama vile “Ukanda Mmoja, Njia Moja”.

Wakati dunia inakabiliwa na changamoto za kudidimika kwa uchumi na  kuongezeka kwa vitendo vya kujilinda kimaslahi vya upande mmoja, China kuendelea kufungua mlango wake, si kama tu kutahimiza maendeleo yake yenyewe, bali pia kutaleta fursa zaidi kwa dunia nzima.