Xi akutana na Putin mjini Moscow
2023-03-21 09:07:18| CRI

Rais Xi Jinping wa China amekutana na mwenzake wa Russia Vladmir Putin katika ikulu ya Kremlin huko Moscow. Xi amesema amefurahi kufanya ziara nyingine nchini Russia ikiwa ni nchi ya kwanza kuitembelea tangu achaguliwe kuwa rais miaka 10 iliyopita na kumbukubu za ziara hiyo zimebaki hadi leo.

Xi amesisitiza kuwa China na Rusia ni majirani wakubwa na washirika wa kina wa kimkakati, na nchi zote mbili zinaupa kipaumbele kikubwa uhusiano wao kwenye diplomasia na sera za mambo ya nje. China siku zote inashikilia sera huru ya mambo ya nje. Kuunganisha na kukuza uhusiano mzuri baina ya China na Russia ni chaguo la kimkakati lililofanywa chini ya maslahi ya kimsingi na mwenendo uliopo duniani.

Aidha kuhusu suala la Ukraine, Xi amesisitiza amani na kusema nchi nyingi zinaunga mkono kuondoa mivutano, kufanya mazungumzo ya amani, na kupinga kuchochea moto. China itaendelea kubeba jukumu la kiujenzi kwenye usuluhishi wa kisiasa wa mgogoro wa Ukraine

Kwa upande wake rais Putin amesema Russia iko tayari kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kivitendo na China, kuongeza mawasiliano na uratibu kwenye masuala ya kimataifa na kuhimiza dunia iwe na mahusiano ya kimataifa yaliyo ya ncha mbalimbali na demokrasia bora zaidi.

Russia inaishukuru China kwa kuendelea kushikilia msimamo wa usawa, wa busara na usio na upendeleo na kusimamia haki na usawa kwenye masuala mengi ya kimataifa. Amebainisha kuwa Russia imeangalia kwa makini waraka wa msimamo wa China kwenye usuluhishi wa kisiasa wa suala la Ukraine na iko wazi kwa mazungumzo ya amani.

Marais hao wawili wamesema wanatarajia mazungumzo rasmi yatakayofanyika leo na kuweka mwongozo mpya kwa uhusiano wa kina na ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Russia katika miaka ijayo.