Tanzania imekuwa mwenyeji wa mkutano wa Kamati ya Kuchakata Data za Hali ya Hewa Duniani, lengo ikiwa ni kuhakikisha data za hali ya hewa zinatumika ipasavyo na taasisi za hali ya hewa katika nchi wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na kwa manufaa ya sekta mbalimbali.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk Hamza Kabelwa amesema, mkutano huo unashirikisha nchi 12 na kueleza kuwa una umuhimu mkubwa kwa nchi.
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk David Richardson, amesema Kamati yake itajikita katika kusaidia kujenga uwezo na kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wote, ili kulinda maisha ya watu na mali zao.