Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesema kuwa serikali yake imefikia hatua muhimu katika usalama wa taifa.
Akizungumza katika uzinduzi wa ofisi mpya ya Mshauri wa Usalama wa Taifa, na Kituo cha Kupambana na Ugaidi cha Kitaifa ambavyo ni vituo viwili vya kisasa vilivyojengwa kwa lengo la kuongeza juhudi za kushughulikia changamoto zinazoendelea za kiusalama, mjini Abuja, rais Buhari amesema serikali yake imeipatia serikali inayokuja miundombinu ya kuratibu ipasavyo masuala ya usalama wa taifa na juhudi za kukabiliana na ugaidi.
Rais Buhari anayetarajiwa kuondoka madarakani Mei 29, amesema maeneo ambayo awali yalikaliwa na magaidi yamekombolewa na wakimbizi wanarejea makwao kwa hiari. Amesema mafanikio hayo yamefikiwa kwa kiasi kikubwa kupitia juhudi shupavu za vikosi vya jeshi na vyombo vingine vya usalama, kwa ushirikiano na washirika wa kikanda na kimataifa.
Mbali na tishio kubwa la ugaidi katika eneo la kaskazini mashariki, ameongeza kuwa serikali imedhibiti msururu wa matukio ya ujambazi wa kutumia silaha na utekaji nyara katika maeneo ya kaskazini magharibi na kaskazini ya kati.