Xi na Putin wasaini taarifa ya pamoja ya Kuimarisha Uhusiano wa Wenzi wa Uratibu wa Kimkakati wa Kina Kwenye Zama Mpya
2023-03-22 09:06:28| CRI

Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Russia Vladimir Putin wamesaini na kutoa taarifa ya pamoja ya marais juu ya Kuimarisha Uhusiano wa Wenzi wa Uratibu wa Kimkakati wa Kina Kwenye Zama Mpya katika ikulu ya Kremlin.

Kwenye taarifa hiyo, pande mbili zimesema uhusiano wa China na Russia sio kama ule wa muungano wa kijeshi na kisiasa wakati wa vita baridi, bali unavuka uhusiano kama huo wa serikali na serikali na hauna asili ya muungano, si wa makabiliano na haulengi upande wowote wa tatu. Zimesema kuwa nchi tofauti zina historia, tamaduni na hali tofauti za kitaifa, na zote zina haki ya kuchagua njia zao za maendeleo. Hakuna kitu kama "demokrasia" bora zaidi.

Kwenye taarifa hiyo Russia imethibitisha kufuata kanuni ya China moja, kuitambua Taiwan kuwa eneo lisiloweza kutengwa la China, kupinga aina yoyote ya Kujitenga kwa Taiwan na kuunga mkono kithabiti hatua za China za kulinda mamlaka na ukamilifu wake wa ardhi.

Halikadhalika pande mbili pia zimeeleza wasiwasi wao mkubwa kuhusu shughuli za kijeshi za kibaolojia za Marekani, ndani na nje ya nchi, ambazo zinatishia pakubwa nchi nyingine na kudhoofisha usalama wa kanda husika. Hivyo wameitaka Marekani kutoa maelezo juu ya suala hili, na kujizuia kuendeleza shughuli zote za kibaolojia ambazo zinakiuka Mkataba wa Silaha za Kibaolojia.

Pande hizo mbili pia zinaitaka Jumuiya ya NATO kufuata ahadi zake kama jumuiya ya kikanda na ya kujilinda, na kuitaka NATO kuheshimu mamlaka, usalama, maslahi pamoja na ustaarabu, historia na utamaduni wa nchi nyingine, na kutafuta maendeleo yao ya amani kwa njia mwafaka. Pia zimeelezea wasiwasi wao mkubwa juu ya kuendelea kwa NATO kuimarisha uhusiano wa usalama wa kijeshi na nchi za Asia na Pasifiki na kudhoofisha amani na utulivu wa kanda hiyo.