Marais wa China na Russia wafanya mazungumzo
2023-03-22 09:03:45| CRI

Rais Xi Jinping wa China amesema yuko tayari kushirikiana na mwenzake wa Russia Vladimir Putin katika kuweka mipango kuhusu uhusiano na ushirikiano wa kivitendo wa pande mbili ili kuhimiza maendeleo na ustawishaji wa nchi hizo mbili.

Rais Xi ameyasema hayo alipozungumza na rais Putin jana mjini Moscow.

Akieleza kuwa China na Russia ni majirani wakubwa zaidi, Xi alisema kuimarisha na kuendeleza uhusiano wa muda mrefu wa ujirani mwema na wa kirafiki na Russia kunaendana na mantiki ya kihistoria na ni chaguo la kimkakati la China, ambalo halitaathiriwa na mabadiliko yoyote yale.

Xi alisema tangu ziara yake ya kwanza ya kiserikali nchini Russia miaka 10 iliyopita, China na Russia zimeheshimiana, kuaminiana na kunufaishana, na uhusiano kati ya nchi hizo mbili upo imara kwa muda wote, na ni wa kina zaidi, kivitendo zaidi na kimkakati zaidi. Alisema bila kujali hali ya kimataifa inavyobadilika, China itaendelea kuhimiza uhusiano wa wenzi wa uratibu wa kimkakati wa pande zote kati yake na Russia katika zama mpya, na kuongeza kuwa ziara yake ya serikali nchini Russia ni safari ya urafiki, ushirikiano na amani.

Kwa upande wake, rais Putin alisema hivi sasa uhusiano kati ya Russia na China umeendelea vizuri na kwamba biashara yao imekua licha ya changamaoto mbalimbali za kimataifa likiwemo janga la COVID-19. Alisema Russia inapongeza China kwa kufanikiwa kuhimiza mazungumzo kati ya Saudi Arabia na Iran mjini Beijing kupata matunda ya kihistoria, jambo ambalo limeonyesha hadhi muhimu na athari chanya ya China ikiwa nchi kubwa duniani. Russia inasifu China kwa kushikilia msimamo wa haki na kutopendelea upande wowote katika masuala ya kimataifa, kuunga mkono mapendekezo yaliyotolewa na China kuhusu usalama, maendeleo na ustaarabu duniani, na kupenda kuimarisha uratibu wa kimataifa na China.

Baada ya mazungumzo yao, marais hao walisaini Taarifa ya Pamoja ya Mpango wa Maendeleo kabla ya mwaka 2030 kwenye Vipaumbele vya Ushirikiano wa Kiuchumi baina ya China na Russia na Taarifa ya Pamoja ya Kuimarisha Uhusiano wa Wenzi wa Uratibu wa Kimkakati wa Kina  Kwenye Zama Mpya.