Peng Liyuan atoa wito wa kuongeza kutoa rasilimali na kushirikiana kwa ajili ya kudhibiti vizuri Kifua Kikuu duniani
2023-03-23 09:05:56| CRI

Mke wa rais wa China, Peng Liyuan ambaye pia ni balozi mwema wa magonjwa ya Kifua Kikuu na Ukimwi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), amezitaka pande zote kuboresha kwa pamoja kinga na matibabu ya kifua kikuu.

Akiongea kwenye hotuba yake ya maandishi kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu Duniani mwaka 2023, Mama Peng amesema pande zote zinapaswa kutekeleza ahadi zao, kuongeza kutoa rasilimali, kuendelea kuwasiliana na kushirikiana, na kupeana uzoefu wa kinga na tiba. Kutokana na kazi kubwa ya WHO na juhudi za pamoja za jamii ya kimataifa, katika miaka ya karibu dunia imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya kifua kikuu.

Mama Peng ameeleza kuwa serikali ya China inatilia maanani sana kinga na tiba ya kifua kikuu na imejumuishwa kwenye mkakati wa afya wa China, ambapo China imekuwa ikiongeza bila kusita kiwango cha kuunga mkono, kuendeleza ushirikiano wa sekta mbalimbali, kushirikisha jamii nzima na kuhimiza kikamilifu mbinu mpya za uchunguzi, ufumbuzi wa tiba na vifaa vya usimamizi, na matokeo yake ni kwamba kiwango cha kutibu kifua kikuu nchini kinaendelea kuwa juu ya asilimia 90.