Qin Gang asema, ziara ya Xi imeonyesha sura ya China kama mjenzi wa amani duniani
2023-03-23 09:02:39| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Qin Gang amesema ziara ya kiserikali aliyomaliza rais Xi Jinping nchini Russia imeonyesha sura ya kimataifa ya China kama mjenzi wa amani, na kudhihirisha nafasi na wajibu wa China kama nchi kubwa duniani, akiongeza kuwa italeta utulivu zaidi katika hali tata ya kimataifa na kusaidia kujenga dunia ya ncha nyingi na kuhimiza ujenzi wa mahusiano ya kimataifa yaliyo ya demokrasia zaidi.

Bw. Qin alisema hayo Jumatano alipozungumza na waandishi wa habari waliofuatana na msafara wa ziara hiyo ya rais Xi nchini Russia. Amesema katika ziara hiyo, rais Xi alisisitiza kuwa China inafuata sera huru ya mambo ya nje ya amani, na daima imekuwa ikifanya maamuzi yake kwa kujitegemea katika msingi wa kuzingatia uhalali wa jambo.

Bw. Qin aliongeza kuwa Katika ziara hiyo, rais Xi na mwenzake Vladimir Putin walifanya mazungumzo ya muda mrefu, ya dhati, ya kirafiki na yenye matunda. Kuhusu suala la Ukraine, taarifa ya pamoja iliyosainiwa na marais hao imesisitiza tena kuwa madhumuni na kanuni ya Katiba ya Umoja wa Mataifa lazima vifuatwe, na sheria za kimataifa lazima ziheshimiwe. Russia imesisitiza tena njia yake ya kurejesha mazungumzo ya amani haraka iwezekanavyo na kuikaribisha China kuchangia kazi za kutatua mgogoro wa Ukraine kwa njia za kisiasa na kidiplomasia.