FAO yapata dola milioni 27 ili kuongeza msaada wa kibinadamu katika eneo la Afrika Mashariki
2023-03-23 22:00:39| cri

Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO) limepata dola za kimarekani milioni 26.9 kwa ajili ya kutoa huduma ya chakula na mahitaji mengine ya kimsingi na huduma kwa watu wanaokabiliwa na ukame katika eneo la Afrika Mashariki.

FAO imesema fedha hizo kutoka Ujerumani zitatumika pia katika kulinda na kurejesha maisha katika jamii zilizoathiriwa zaidi na ukame nchini Ethiopia, Kenya, Somalia na Sudan. Taarifa imesema fedha hizo ni mchango mkubwa katika kupunguza athari za ukame kwa usalama wa chakula na maisha, kwa kuwa utaongeza upatikanaji wa chakula katika jamii za vijijini, kulinda na kurejesha maisha, na kuziwezesha jamii hizo kujitegemea haraka.

Kutokana na mazao kutoota vizuri, wanyama wanakufa, na idadi kubwa ya watu wamehama makazi yao. Ukame mkali umesababisha uhaba mkubwa wa chakula katika eneo la Afrika Mashariki, huku zaidi ya watu milioni 22 kusini mwa Ethiopia, Kenya, na Somalia wakihitaji msaada wa dharura.