UNECA yasema nchi 10 za Afrika kukabiliwa na kiwango kikubwa cha umasikini
2023-03-23 21:59:56| cri

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Kamati ya Uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa na Mchumi Mwandamizi wa Kamati hiyo, Hana Morsy amesema, nchi 10 za Afrika zinakabiliwa na kiwango kikubwa cha umasikini katika bara hilo.

Akizungumza katika kikao cha 55 cha ngazi ya mawaziri cha Mkutano wa Kamati ya Uchumi wa Afrika wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi mjini Addis Ababa, Ethiopia, Morsy amezitaja nchi hizo kuwa ni Burundi, Somalia, Madagascar, Sudan Kusini, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Malawi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Guinea-Bissau, Msumbiji na Zambia.

Akinukuu utafiti uliofanywa na UNECA, Morsy amesema katika kila nchi hizo 10, kati ya asilimia 60 na 82 ya watu wake ni masikini, na kwamba UNECA inakadiria kuwa familia katika bara la Afrika zinatumia asilimia 40 ya kipato chao kwa chakula, na migogoro inayoendelea duniani imeziathiri zaidi familia masikini zaidi barani Afrika.

Ameongeza kuwa, kuna kiwango kikubwa cha umasikini na ukosefu wa usawa wa kijinsia barani Afrika, hata kabla ya migogoro inayoshuhudiwa duniani, lakini hivi sasa umasikini umeongezeka, na kuna pengo kubwa katika ukosefu wa usawa wa kijinsia.