Taasisi ya Confucius nchini Djibouti ilifunguliwa rasmi jana huku wadau mbalimbali wakiahidi kuifanya taasisi hiyo kuwa jukwaa bora la kuimarisha ushirikiano kati ya China na Djibouti.
Akihutubia sherehe ya ufunguzi wa taasisi hiyo, waziri wa elimu na Mafunzo ya Ufundi wa Djibouti Bw. Moustapha Mohamed Mahamoud, amesema Djibouti inatambua umuhimu wa lugha ya Kichina kuwa jukwaa la kuimarisha ushirikiano wa pande zote kati ya China na Djibouti. Amesisitiza matumaini yake kwamba taasisi hiyo itaongeza zaidi uhusiano wa kitamaduni na mawasiliano kati ya watu na watu wa nchi hizo mbili.
Balozi wa China nchini Djibouti Hu Bin ameeleza imani yake kuwa kujifunza lugha na tamaduni za kila upande, kunasaidia kuinua uhusiano kati ya nchi hizo mbili, na kuwa China iko tayari kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na Djibouti.