Uganda imetoa tahadhari ya maafa ikisema, wakati msimu wa kwanza wa mvua unaanza, baadhi ya sehemu za nchi hiyo zitakabiliwa na mafuriko, maporomoko ya udongo, maporomoko ya matope ya mvua, na mvua ya mawe na radi.
Waziri wa Nchi anayeshughulikia Misaada, Utayari wa Maafa na Wakimbizi wa Uganda Bi. Esther Anyakun amesema, mikoa ya Mashariki, Katikati na Magharibi nchini humo na bonde la Ziwa Victoria zitakabiliwa na mvua kubwa itakayozidi kiasi cha kawaida hadi mwezi Mei, ambayo huenda ikasababisha kuharibika kwa mashamba na mazao, na kuongezeka kwa magonjwa yanayotokana na maji kama vile homa ya matumbo, kipindupindu na malaria.
Alisema serikali inasambaza ujumbe wa tahadhari mapema, na kujenga uwezo wa watu binafsi, jamii na taasisi ili kupunguza hatari na kuongeza ustahimilivu zaidi.