Waziri wa mambo ya nje wa China akutana na mwenzake wa Guinea ya Ikweta
2023-03-24 09:18:43| CRI

Waziri wa Mambo ya Nje wa China Bw. Qin Gang jana alikutana na mwenzake wa Guinea ya Ikweta Bw. Simeon Oyono Esono Angue mjini Beijing.

Bw. Qin aliahidi kuwa China itaiunga mkono kithabiti Guinea ya Ikweta katika kutafuta kwa uhuru njia ya maendeleo inayoendana na hali yake ya kitaifa, kulinda mamlaka ya kitaifa na kupinga uingiliaji wa nje katika mambo yake ya ndani. Amesema nchi hizo mbili zinapaswa kuzingatia makubaliano muhimu yaliyofikiwa na wakuu wa nchi hizo mbili, kudumisha mawasiliano ya hali ya juu, kuimarisha ushirikiano wa kivitendo, kuzidisha mawasiliano ya kiutamaduni na baina ya watu, na kuunganisha uungaji mkono wa umma ili kuendeleza uhusiano wa pande hizo mbili. Ameongeza kuwa makampuni ya biashara ya China yanahimizwa kuwekeza nchini Guinea ya Ikweta na soko la China linakaribisha bidhaa zaidi kutoka Guinea ya Ikweta.

Kwa upande wake, Bw. Esono Angue amesema China ni rafiki wa kweli, ndugu mwema na mwenzi mzuri wa Guinea ya Ikweta na Afrika, na hakuna chochote kinachoweza kuzuia kuimarisha urafiki na ushirikiano na China. Ameongeza kuwa Guinea ya Ikweta inafuata kithabiti kanuni ya China moja na kupinga kuingilia masuala ya ndani ya China kwa kisingizio cha haki za binadamu.