Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inatarajia kuzindua ujenzi wa makao makuu mapya ya jumuiya hiyo jijini Arusha kwenye eneo la ekari 125 lililotolewa na serikali ya Tanzania.
Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Bw. Peter Mathuki amesema kwa sasa wanatafuta ufadhili kwa ajili ya ujenzi wa eneo hilo.
Bw. Mathuki amesema wanatafuta wataalamu wa ufundi kutoka nchi wanachama ili kuja na mpango wa uendelezaji wa eneo la Kisongo lililopo nje kidogo ya mji wa Arusha, nje ya barabara ya kuelekea Dodoma.
Jumuiya ya Afrika Mashariki ina idara na taasisi 12, huku Arusha yakiwa ni makao makuu ya sekretarieti.
Bunge la Afrika Mashariki, Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki na Mamlaka ya Ushindani ya Afrika Mashariki, ambayo makao yake makuu bado hayajapangiwa mahali, yapo katika makao makuu ya jumuiya hiyo kwa muda.
Makao makuu ya idara nyingine tisa yako kwenye nchi mbalimbali washirika. Tanzania na Uganda ni wenyeji wa idara zaidi ya moja, huku Kenya, Rwanda na Burundi zikiwa ni wenyeji wa idara moja kila moja.