Shirika la Maendeleo ya Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) limeomba msaada wa dola za kimarekani bilioni 2.69 ili kuokoa maisha ya watu walio hatarini kukabiliwa na njaa katika nchi za Kenya, Uganda na Somalia kutokana na ukame.
Katibu Mkuu wa IGAD, Workneh Gebeyehu amesema, hali inaendelea kuwa mbaya, na watu milioni 47 wanakabiliwa na ukosefu wa usalama wa chakula na wako hatarini kufa kutokana na njaa.
Shirika hilo limesema Somalia inahitaji dola bilioni 1.6 za kimarekani kutoa bidhaa za chakula na zisizo za chakula kwa jamii zilizoathiriwa na ukame na wakimbizi wa ndani, huku Ethiopia ikihitaji dola za kimarekani milioni 710 kusaidia mahitaji muhimu katika miezi minne ijayo, na Kenya inahitaji dola za kimarekani milioni 378 kutoa msaada wa chakula, maji, na chanjo kwa kaunti zilizoathiriwa mpaka mwezi Oktoba.