Waziri Mkuu wa Tanzania asema serikali inataka viwango vya riba ya mikopo vipunguzwe
2023-03-28 20:01:27| cri

Waziri Mkuu wa Tanzania Bw. Kassim Majaliwa amesema serikali inajadiliana na taasisi za fedha za ndani kuhusu uwezekano wa kupunguza riba za mikopo na makato mengine katika jitihada za kuwavutia wananchi wengi zaidi kwenye sekta ya benki.

Akiongea kwenye uzinduzi wa tawi jipya la Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) mjini Bariadi, mkoani Simiyu Bw. Majaliwa amesema kuna wananchi ambao wanaogopa kuchukua mikopo katika taasisi za fedha za uhakika kutokana na viwango vya juu vya riba na makato mengine yanayotozwa na taasisi hizo za fedha.

Amesema tayari serikali imezungumza na taasisi za fedha, na taasisi hizo zimeanza kulifanyia kazi haraka suala hilo. Bwana Majaliwa pia ameiomba benki ya NBC kuhakikisha kuwa inafungua fursa zaidi za uzalishaji na kukuza uchumi hasa kupitia sekta ya biashara, kilimo na mifugo.