Xi azungumza kwa njia ya simu na mwanamfalme na waziri mkuu wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman
2023-03-28 14:45:12| cri

Rais Xi Jinping wa China leo amezungumza kwa njia ya simu na mwanamfalme na waziri mkuu wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.

Rais Xi amesema China inapenda kuendelea kuungana mikono na Saudi Arabia katika masuala yanayohusu maslahi ya msingi ya upande mwingine, kupanua ushirikiano wa kivitendo na mawasiliano ya kitamaduni, kuendeleza zaidi uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Saudi Arabia, kujenga jumuiya ya China na nchi za kiarabu yenye mustakabali wa pamoja katika zama mpya, na kutoa mchango zaidi kwa ajili ya amani, utulivu na maendeleo katika Mashariki ya Kati.

Xi Jinping amesema kutokana na juhudi za pamoja za China, Saudi Arabia na Iran, mazungumzo kati ya Saudi Arabia na Iran yaliyofanyika hivi karibuni mjini Beijing yamepata mafanikio makubwa, ambayo yatasaidia kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili, na kutoa mfano mkubwa wa kuigwa kwa nchi za kanda hiyo kuimarisha mshikamano na ushirikiano na kutatua mivutano yao kwa njia ya mazungumzo.

Kwa upande wake, Mohammed amesema Saudi Arabia inaishukuru China kwa juhudi zake za kuboresha uhusiano kati ya Saudi Arabia na Iran, ambazo zimeonyesha sura ya China ya nchi kubwa inayowajibika. Pia ameipongeza China kwa kufanya kazi muhimu za kiujenzi katika masuala ya kikanda na kimataifa, na Saudi Arabia inatilia maanani kuendeleza uhusiano na China, na inapenda kushirikiana na China katika kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.