Kama ambavyo amesema Pili, kipindi hiki cha Ukumbi wa Wanawake kinajadili masuala mbalimbali yanayomhusu mwanamke, mtoto, na hata kijana. Mwanamke mara nyingi anachukuliwa kama kiumbe dhaifu, kiumbe asiye na uwezo wa kufanya mambo makubwa, lakini katika miaka ya karibuni, wanawake wameibuka na kuwa vinara wa kufanya mambo makubwa, hata katika zile kazi ambazo awali ziliaminika kuwa ni za wanaume.
Ni kweli, kwani katika kipindi hiki cha Ukumbi wa Wanawake tumezungumzia mafanikio mengi ambayo wamepata wanawake katika maeneo mbalimbali. Wanawake wameendelea kufanya vizuri katika uongozi, katika biashara, katika sekta ambayo tunasema ngumu, ya sayansi na teknolojia, na pia kuna wanawake wahandisi ambapo wameendelea kupasua anga na kujipatia umaarufu mkubwa katika sekta husika.
Kwa kifupi tunaweza kusema zile zama za kusema kuwa, mwanamke nafasi yake ni jikoni na kulea familia, zimepitwa na wakati. Ni kweli, bado mama ana jukumu la kulea familia, lakini pia ana fursa ya kuonyesha kipawa chake katika maeneo mbalimbali. Hivyo basi, katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake leo hii, tutaendelea kuangalia mafanikio na changamoto wanazokumbana nazo wanawake katika utekelezaji wa majukumu yao.