Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amerejea tena ahadi ya dunia ya kushikamana na Afrika katika mapambano dhidi ya ugaidi, huku akionya kuwa njia ya ugaidi inaendelea kuwa pana katika bara hilo.
Akizungumza katika mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu kukabiliana na ugaidi kwa kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja huo na mashirika ya kikanda, Guterres amesema, hakuna umri, dini, utaifa, na kanda ambayo haikuwa hatarini, na kuongeza kuwa hali barani Afrika inaleta wasiwasi zaidi.
Amesema kukata tamaa, umasikini, njaa, ukosefu wa huduma za msingi, ukosefu wa ajira na mabadiliko yaliyofuata katika serikali vimeendelea kuweka mazingira mazuri ya kuongezeka kwa makundi ya kigaidi yanayoingia katika maeneo mapya barani Afrika.