Panya Buku waliopata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) wanatumika kutambua sampuli zaidi ya 100 za vimelea vya ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) kwa dakika 20. Panya hao wanaopatikana kwenye maabara za APOPO Dar es Salaam na SUA Morogoro, huweza kutambua vimelea vya TB kwenye makohozi kwa kasi kubwa kiasi kuliko wataalamu wa maabara ambao wanatumia siku nne kuchunguza idadi hiyo ya sampuli.
Maabara za APOPO hukusanya sampuli kutoka kwenye vituo vinavyopima TB kwa ajili ya mafunzo kwa Panya, lakini pia kwa utambuzi zaidi ili kubaini uwepo wa vimelea hivyo vya TB. Mratibu wa Kifua Kikuu, Mkoa wa Dar es Salaam Mbarouk Seif Khaleif amesema Panya hao hupewa mafunzo na wana uwezo wa kunusa na kutambua kwa haraka vimelea vya ugonjwa wa TB. Mfumo huu wa kutumia panya kutambua TB ulianzishwa na shirika la misaada Ubelgiji, kama njia nyepesi na isiyotumia fedha nyingi kutambua TB kinyume na mfumo uliozoeleka.
Dk Mbarouk anasema Dar es Salaam ndio inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi wa TB huku, takwimu za Wizara ya Afya zilizotolewa Machi 24, zinaonyesha kuwa watu 71 hufariki kila siku nchini Tanzania kutokana na TB.