Idadi ya vifo kutokana na kimbunga cha kitropiki “Freddy” nchini Malawi huenda ikazidi 1,200
2023-03-31 21:02:15| cri

Kimbunga cha kitropiki “Freddy” kiliikumba Malawi tarehe 13 Machi. Hadi kufikia tarehe 29 Machi, watu wasiopungua 676 walifariki dunia kutokana na mvua kubwa na maporomoko ya udongo vilivyosababishwa na kimbunga, na wengine 538 hawajulikani walipo.

Idara ya Menejimenti ya maafa ya Malawi imesema hakuna uwezekano mkubwa wa kuwapata watu hao 538 wasiojulikana walipo baada ya wiki mbili tangu maafa yalipotokea. Hivyo idadi ya vifo kutokana na kimbunga hicho “Freddy” nchini humo huenda ikazidi 1,200.

Msemaji wa polisi ya Malawi amesema polisi na askari wanaendelea kuwatafuta watu hao, baada ya mchakato huo kumalizika, wale ambao bado hawatapatikana watatangazwa kufariki dunia.