Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani inayotokea katika sehemu ya shingo ya uke ambapo sell za kansa hujiunda na kusababisha kizazi kupata madhara katika afya ya uzazi. Aina hii ya saratani inaongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi duniani, na inakadiriwa kuwa, asilimia 85 ya vifo hivi hutokea katika nchi zinazoendelea. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (W.H.O) ya mwaka 2010, nchini Tanzania, wastani wa wanawake 6,241 huugua saratani hii kila mwaka, ambapo 4,355 kati yao hufa.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, mwaka jana pekee, ni asilimia 13 tu ya watoto wa kike wenye umri wa miaka 9 hadi 14 duniani walipewa chanjo ya HPV ambayo inasababisha saratani hiyo. Dr. Ghebreyesus ameungana na watu mbalimbali mashuhuri, wake za marais, manusura wa saratani hiyo na jumuiya za mashirika na wadau wa afya katika kampeni ya kimataifa ya kutokomeza saratani hiyo. Kutokana na tatizo hili kuendelea kuwatesa wanawake n ahata wasichana, katika kipindi chetu cha leo cha Ukumbi wa Wanawake, tutazungumzia zaidi saratani ya shingo ya uzazi, nani wako hatarini kupata saratani hii, kama inatibika, na ni kwa njia gani wanawake na wasichana wanaweza kuepukana na saratani hii.