Chama tawala cha Rwanda (Rwandan Patriotic Front-Inkotanyi) kimeadhimisha miaka 35 tangu kuanzishwa kwake.
Mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa Rwanda Bw. Paul Kagame, amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji na kujitolea ili kukiendeeza chama hicho na kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika miongo iliyopita.
Akizungumza kwenye mkutano mkuu wa 16 wa chama hicho kwenye makao makuu yake katika ukumbi wa mikutano wa Intare mjini Kigali, Rais Kagame amesema tangu mwanzo, chama hicho kilichagua kanuni tatu ambazo ni kufikiria mambo makubwa, kufanya kazi kwa pamoja, na kuwajibika.
Amesema Rwanda na RPF wana viwango sawa vya malengo, matarajio, hisia ya uwajibikaji, na kubeba mzigo kama nchi nyingine yoyote, bila kujali ukubwa wake.