Trump ashtakiwa kwa makosa 34 ya kugushi rekodi za biashara, mwenyewe akana mashtaka
2023-04-05 08:33:32| CRI

Aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump ameshtakiwa kwa makosa 34 ya kugushi rekodi za biashara, na kufikishwa katika Mahakama ya makosa ya Jinai ya Manhattan Jijini New York, na kuwa mtu wa kwanza aliyekuwa rais wa Marekani kushtakiwa kwa makosa ya jinai.

Mwanasheria wa wilaya ya Manhattan Bw. Alvin Bragg alitangaza mashtaka hayo baada ya Bw. Trump kufikishwa mahakamani, akimtuhumu kwa kugushi rekodi za biashara za New York, ili kuwaficha wapiga kura wa Marekani taarifa mbovu na shughuli zisizo halali kabla na baada ya uchaguzi wa 2016.

Bw. Bragg amesema wakati wa uchaguzi, Bw. Trump na wenzake wengine walitumia mpango wa "kamata na kuua" kutambua, kununua, na kuficha habari mbaya kumhusu yeye na kuongeza matarajio yake ya uchaguzi.

Bw. Trump amekanusha mashtaka na kusema kuwa uchunguzi wa uhalifu unaoongozwa na Bw. Bragg, ambaye ni mwanachama wa Democrat, unachochewa kisiasa.