China na Tanzania zawakumbuka wataalamu wa China waliokufa kwenye mradi wa TAZARA
2023-04-05 08:35:49| CRI

Maofisa waandamizi wa serikali ya Tanzania wamejiunga na jumuiya ya Wachina wanaoishi nchini humo kwenye hafla ya Siku ya Kusafisha Makaburi ya China kwa ajili ya kuwakumbuka wataalamu waliofariki dunia kwenye ujenzi wa Reli ya TAZARA na katika utekelezaji wa miradi mingine ya ushirikiano kati ya China na Tanzania.

Hafla hiyo ya kumbukumbu ilifanyika katika Eneo la Makaburi ya Wataalamu wa China huko Pugu. Akiongea kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Atupele Mwakibete amesema, wakati wakiangalia mafanikio ya mradi huu mkubwa wa uhandisi uliotekelezwa na China barani Afrika katika miaka ya 70 ya karne ya 20, hawapaswi kuwasahau wale waliopoteza maisha kwa ajili ya mradi huo.