EAC yaipongeza Rwanda kwa kuendeleza umoja na maridhiano baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994
2023-04-10 08:58:40| CRI

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeipongeza Rwanda kwa kukuza umoja na maridhiano baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Peter Mathuki mjini Arusha, Tanzania, ijumaa jioni katika kumbukumbu ya miaka 29 ya Mauaji ya Kimbari dhidi ya Watutsi imesema, miaka 29 baada ya mauaji hayo, Rwanda imepiga hatua kubwa kupita matarajio ya wengi, na inapaswa kupongezwa kwa mafanikio hayo.

Amesema wakati dunia ikikumbuka mauaji hayo, ni muhimu kurejea tena ukweli wa kimsingi kuwa, binadamu wote wameumbwa kwa usawa, kila mmoja ana haki za kimsingi zisizopingwa, ikiwemo haki ya kuishi, na kuongeza kuwa, hakuna mtu mwenye haki ya kutoa maisha ya mwingine kama ilivyofanyika miaka 29 iliyopita.