Tamthiliya, mashairi, nyimbo na maonyesho mbalimbali ya wasanii vijana wa Rwanda yamefanyika mjini Kigali ili kuwakumbusha vijana kuhusu historia ya mauaji ya kimbari yaliyotokea mwaka 1994.
Maonyesho hayo ni sehemu ya kumbukumbu ya miaka 29 ya mauaji ya halaiki iliyoanza Aprili 7, yakiwa na lengo la kuwapa vijana ukweli kuhusu historia ya mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi, ili kusaidia kukabiliana na wanaokana mauaji ya kimbari na kuchangia katika ujenzi wa amani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Vijana ya Rwanda Bwana Parfait Busabizwa, amesema kwenye maonyesho hayo, kuwa vijana wana nafasi nzuri zaidi ya kulinda umoja wa Wanyarwanda na kutumia rasilimali za kidijitali za mitandao ya kijamii kufahamisha ukweli halisi kuhusu mauaji ya kimbari.
Viongozi mbalimbali waliohutubia maonyesho hayo wamewaelimisha vijana kuhusu chanzo cha mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, na jinsi yalivyositishwa na Jeshi la RPF la Rwanda.
Takriban vijana 2,000 na maofisa wa serikali waliohudhuria shughuli hiyo waliwasha mishumaa kuwakumbuka wahanga wa mauaji.