Kuanzia Machi 23 yaani siku ya Jumatano, Waislamu kote duniani walianza kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani. Katika kipindi hiki Waislamu huwa wanajiegemeza zaidi kwenye sala na ibada ikiwemo kujizuia mambo yote yaliyokatazwa yakiwa ni pamoja na kula na kunywa wakati wa mchana, na kuomba msamaha kwa makosa yao waliyoyafanya. Lakini mbali na ibada, katika kipindi hiki pia huwa tunashuhudia wanawake wakipirikika huku na kule kuandaa mapishi ya aina mbalimbali kwa ajili ya futari.
Kawaida kila mwislamu duniani anajiandaa mapema kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Waislamu wa Beijing nao halikadhalika wana taratibu zao mbalimbali za kuukaribisha mwezi katika kipindi hiki. Mimi na mwenzangu tumeishi Beijing kwa muda mrefu sana na kuonja karibu mapishi mengi ya Beijing na ya miji mingine, Hivyo leo katika kipindi hiki cha Ukumbi wa Wanawake tutaangalia mapishi ya Beijing ama vyakula maarufu vya Beijing ambavyo Waislamu huwa wanakula katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani, na pia tutaangalia uzoefu wa wageni Waislamu ambao wapo hapa China kimasomo.