UM wasema vitisho vya kuuawa havijaathiri operesheni za misaada za Umoja huo nchini Sudan
2023-04-12 08:36:42| CRI

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema, Umoja huo haujasitisha operesheni zake za kutoa misaada licha ya mtu mmoja kutaka idhini ya kumuua mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan.

Akizungumza na wanahabari hapo jana, Dujarric ameeleza wasiwasi mkubwa juu ya video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii, ikimwonyesha mwanaume mjini Khartoum akiomba fatwa kumruhusu kumuua Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Volker Perthes, bila ya kutaja sababu za kutaka kufanya hivyo.

Dujarric amesema, serikali ya Sudan inawajibika na ina jukumu la kuhakikisha usalama wa Tume ya Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wake wote, kama ilivyoelekezwa kwenye makubaliano ya mwaka 2021 kati ya Umoja wa Mataifa na serikali ya Sudan.