Utafiti mazao ya bahari kumaliza tatizo la mbegu, chakula
2023-04-12 19:58:39| cri

Wakati ukizinduliwa mradi wa utafiti wa mazao ya bahari, mazingira na maliasili kukuza uchumi wa buluu, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amesema kuna tatizo sugu la kufanya tafiti zinazoishia kwenye makaratasi na kuonya jambo hilo lisitokee katika mradi huo.

Mradi huo uliobuniwa na Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza) kwa udhamini wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), unalenga kutoa suluhisho kwa wavuvi na wakuzaji wa viumbe wanaokumbana na tatizo la mbegu na chakula.

Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo Aprili 11, 2023 katika Chuo cha Suza Kampasi ya Nkrumah Unguja, Hemed alisema tafiti zinazoishia maktaba bila kusambazwa huwa zinaitia hasara Serikali.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk. Amos Nungu amesema walipata maandiko 75 kuhusu uanzishaji wa mradi huo na Suza kuibuka mshindi ambapo mradi huo utakuwa kichocheo kikubwa katika sera ya Serikali kuhusu uchumi wa buluu.