Katibu Mkuu wa UM atoa wito wa uungaji mkono wa dharura wa kibinadamu ili kuzuia mgogoro nchini Somalia
2023-04-13 08:27:23| CRI

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amemaliza ziara yake ya siku mbili nchini Somalia kwa kutoa wito kwa wafadhili kuongeza msaada wa kibinadamu ili kuzuia mgogoro nchini Somalia, ambayo bado inakabiliwa na tishio la baa la njaa.

Guterres aliyewasili Somalia Jumanne wiki hii, amesema kuna haja ya kuchukua hatua sasa ili kuzuia janga hilo linalotokana na ukame mkali unaoendelea nchini Somalia. Ameongeza kuwa, kati ya sasa mpaka mwezi Juni mwaka huu, Wasomali milioni 6.5 wako hatarini kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Amesema hali ya sasa bado inaleta wasiwasi, na kuongeza kuwa, mabadiliko ya tabianchi yanasababisha mgogoro nchini Somalia, ambako uhaba mkubwa wa mvua umeshuhudiwa kwa misimu mitano.

Guterres pia amempongeza rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud kwa juhudi zake za kuendeleza amani na usalama, na kuonyesha umuhimu wa uratibu zaidi serikali kuu katika kukabiliana na tishio linaloletwa na kundi la al-Shabab.