Marekani yapaka matope China katika suala la madeni barani Afrika
2023-04-13 14:34:04| CRI

Hivi karibuni, tatizo la madeni barani Afrika limefuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa. Marekani imetumia fursa hii kuikashifu China kuwa kikwazo cha utatuzi wa madeni ya nchi za Afrika. Lakini ukweli ni kwamba, China imetoa mchangao zaidi katika suala la madeni ya nchi za Afrika, jambo ambalo Marekani inapaswa kufanya, ni kuwajibika katika suala hilo.

Kulingana na takwimu, katika miaka mitatu ijayo, jumla ya malipo ya madeni ya nchi za Afrika yatakuwa dola bilioni 106 za kimarekani, hali ambayo itaathiri nchi nyingi za Afrika ikiwemo Zambia. Kuanzia mwezi Novemba mwaka 2020, Zambia ilianza kuwa na dalili ya msukosuko wa madeni, ikishindwa kulipa deni la Euro milioni 42.5. Hivi sasa, nchi hiyo ina mzigo mkubwa wa madeni ya nje ambayo yamefikia dola bilioni 17 za kimarekani. Kwa kuwa China imefanya uwekezaji zaidi nchini Zambia, Marekani inadai kuwa China ni chanzo cha msukosuko wa madeni nchini humo. Mwanzoni mwa mwaka huu, Waziri wa Fedha wa Marekani Jenet Yellen alichagua kwa makini nchi tatu za Afrika alizotembelea, ikiwa ni pamoja na Zambia. Katika ziara hiyo, Yellen aliipaka matope China katika suala la madeni ya Afrika, na kusema kama angeweza kufanya ziara nchini China, jambo la kwanza analopenda kujadiliana na China ni suala la madeni ya nchi zinazoendelea.

Lakini ukweli ni kwamba, China inajitahidi sana kuzisaidia nchi za Afrika kushughulikia tatizo la madeni, na miongoni mwa Kundi la Nchi 20 (G20), China imetoa mchango mkubwa zaidi katika juhudi za kuahirisha na kupunguza malipo ya madeni ya nchi za Afrika. Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na Taasisi ya Utafiti wa Mambo ya China na Afrika ya Chuo Kikuu cha John Hopkins nchini Marekani inaonyesha kuwa, China imeshiriki kwa hatua madhubuti zaidi katika mpango wa G20 wa kuahirisha na kupunguza madeni ya nchi zinazoendelea, na kuchangia asilimia 63 ya mpango huo. Ripoti hiyo inasema, China imefanya mawasiliano mazuri na nchi za Afrika katika suala la madeni, na kutekeleza vizuri majukumu yake.

Kuhusu msukosuko wa madeni barani Afrika, Marekani yenyewe inapaswa kubeba jukumu kuu. Kwanza ni sera yake ya fedha. Ili kukabiliana na mfumuko wa bei, Marekani hivi karibuni imepandisha viwango vya riba mara nyingi, hatua ambayo imeleta athari kubwa kwa nchi za Afrika, ikiwemo Zambia, kwani nchi hizo zitalipa riba kubwa zaidi kutokana na mzigo mkubwa wa madeni. Pili, katika nchi nyingi za Afrika, wakopeshaji wakubwa zaidi ni mashirika ya kibiashara ya nchi za Magharibi na mashirika ya kimataifa. Mashirika hayo ambayo mengi yanamilikiwa na Marekani, yanachukua karibu robo tatu ya madeni ya jumla barani Afrika. Lakini Marekani inakaa kimya kuhusu hali hii, na kukataa ombi la China la kuhusisha wakopeshaji wa kibiashara na mashirika ya kimataifa katika juhudi za kutatua suala la madeni ya Afrika.

Mara kwa mara Marekani inalaumu China kuhusu suala la madeni barani Afrika. Wengi wanajiuliza, je, kitendo hicho ni kwa ajili ya Afrika kweli? Jibu ni hapana. Marekani inatumia suala hilo kama silaha yake ya kushindana na China.

Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imezidi kuiona China kama mshindani wake mkubwa, na Afrika imekuwa moja ya maeneo muhimu ya kushindana na China. Mwaka jana, Rais wa Marekani Joe Biden alikusanya viongozi wa nchi 49 za Afrika mjini Washington, na kutangaza atatoa uwekezaji wa dola bilioni 55 za kimarekani barani Afrika. Hata hivyo, ahadi za Marekani mara kwa mara zimekuwa ni maneno matupu. Wakati wakiwa madarakani, marais Barack Obama na Donald Trump walitoa ahadi za kiuchumi kwa nchi za Afrika, kama vile kupanua biashara na Afrika na kuzisaidia nchi za Afrika kuongeza uzalishaji wa umeme, lakini ahadi hizo hazikutimizwa.

Kwa Marekani, njia ya bei nafuu zaidi ni kuutenganisha uhusiano kati ya China na Afrika, kwa kuipaka matope China katika masuala mbalimbali ya Afrika, ikiwemo suala la madeni.