Huu ni mwaka wa kumi tangu Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia Moja” litolewe. Katika muongo uliopita, ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika chini ya pendekezo hilo umezaa matunda mengi. Msomi wa Nigeria Dkt. Michael Ehizuelen amesema, ushirikiano wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” umeinua kwa kiasi kikubwa kiwango cha miundombinu barani Afrika, na kutoa mchango mkubwa katika kusukuma mbele muunganiko wa kikanda na mafungamano ya kiuchumi ya Afrika.
Dkt. Ehizuelen, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa kituo cha utafiti wa Nigeria cha Taasisi ya Utafiti wa Afrika katika Chuo Kikuu cha Ualimu cha Zhejiang, amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni, kutokana na kupigwa jeki na ushirikiano wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja”, muunganiko wa miundombinu kati ya nchi za Afrika umepiga hatua kwa kasi, ambapo reli ya Addis Ababa-Djibouti, reli ya SGR ya Nairobi-Mombasa na miradi ya awamu ya kwanza na ya pili ya kuifanya reli iwe ya kisasa nchini Nigeria imekamilika kwa nyakati tofauti na kuanza kutoa huduma kwa umma. Amesema, kuboreka kwa miundombinu ya reli kumesukuma mbele kidhahiri biashara kati ya nchi za Afrika na kuhimiza mafungamano ya kiuchumi ya kikanda. China pia imeshirikiana na nchi za Afrika katika kujenga maeneo ya ushirikiano wa kiuchumi, maeneo maalumu ya kiuchumi na kadhalika, ambayo yamevutia makampuni kutoka China na nchi nyingine kuwekeza na kujenga viwanda barani Afrika, hatua inayoharakisha maendeleo ya viwanda barani humo na kufungua uwezo wa maendeleo ya kiuchumi.
Dkt. Ehizuelen akitolea mfano wa mradi wa reli ya kisasa ya SGR kutoka Abuja hadi Kaduna nchini Nigeria uliojengwa na kampuni ya China, amesema kuwa reli hiyo imeleta mabadiliko chanya kwa maisha ya watu wa huko. Reli imechochea maendeleo ya uchumi wa maeneo inayopita, ambako masoko na mahoteli mengi yamejengwa, na hivyo kutoa nafasi nyingi za ajira. Dkt. Ehizuelen amesema kwenye kituo cha treni cha Rigasa ambacho ni cha mwisho katika reli hiyo, aliwahi kufanya mahojiano na dereva wa lori Bw. Musa Usman, ambaye alianzisha kampuni yake ya uchukuzi ndani ya miaka miwili kutokana na kuongezeka kwa wasafiri na mizigo inayoletwa na reli ya Abuja-Kaduna.
Dkt. Ehizuelen anaona, reli ya Abuja-Kaduna ni mfano mmoja tu wa jinsi ushirikiano wa “Ukanda Mmoja, Njia Moja” unavyohimiza maendeleo ya Afrika na kuleta manufaa halisi kwa maisha ya watu wa Afrika. Amesema, yaliyoletwa na “Ukanda Mmoja, Njia Moja” ni msukumo wa kupiga jeki uchumi na kuzisaidia nchi za Afrika kugeuza raslimali zake kuwa maendeleo halisi.