UM waonya kuhusu mlipuko wa magonjwa yanayotokana na maji nchini Somalia kufuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha
2023-04-14 08:37:20| CRI

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, mafuriko ya ghafla na kufurika kwa mito kunakotokana na mvua kubwa nchini Somalia kunaweza kusababisha milipuko ya magonjwa yanayotokana na maji.

Ofisi hiyo imesema, mvua hizo zimekuja wakati mlipuko wa kipindupindu na kuhara umeripotiwa katika mkoa wa Jubaland, kusini mwa Somalia, na mkoa wa Kusini Magharibi. Ikinukuu takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya ya Somalia, OCHA imesema karibu kesi 4000 zinazoshukiwa kuwa na kipindupindu na vifo 17 vinavyohusishwa na ugonjwa huo vimeripotiwa katika wilaya 27 nchini humo tangu mwezi Januari.

OCHA imesema, maeneo yaliyoathiriwa zaidi na mafuriko ni wilaya ya Bardhere mkoani Gedo, kusini mwa Somalia, na wilaya ya Baidoa iliyoko mkoa wa Bay, kusini magharibi mwa Somalia.