Mfumuko wa bei nchini Tanzania kwa mwezi Machi, mwaka huu umepungua hadi asilimia 4.7 kutoka asilimia 4.8 ya mwezi Februari.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema kupungua kwa mfumuko wa bei kunaonesha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa kwa mwezi Machi imepungua kidogo ikilinganishwa na Februari.
Akiongea na wanahabari mjini Dodoma, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa alisema mfumuko wa bei ulipungua mwezi Machi kutokana na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula zikiwemo mchele ambao bei yake ilishuka kutoka asilimia 32.7 hadi asilimia 32, unga wa ngano bei ilipungua kutoka asilimia 18.8 hadi asilimia 16.1, unga wa mtama kutoka asilimia 5.8 hadi asilimia 5.6 na matunda ambayo bei imepungua kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 7.4 na vilevile bidhaa zisizo za vyakula katika kipindi hicho.
Aidha, Dk Chuwa alibainisha kuwa mfumuko wa bei wa Tanzania umepungua kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki, ambapo katika kipindi hicho, mfumuko wa bei wa Uganda umepungua kutoka asilimia 9.2 hadi asilimia 9.0, huku Kenya, ukibaki asilimia 9.2.