China yaisaidia Tanzania kuboresha uwezo wa uhifadhi wa maji katika Maziwa Makuu
2023-04-14 08:36:39| CRI

China imefanya semina ya siku mbili inayolenga kuisaidia Tanzania kuongeza uwezo wake wa uhifadhi na usimamizi wa maji katika Maziwa Makuu ya nchi hiyo.

Semina hiyo ya mafunzo kuhusu Mazingira ya Ikolojia na Usalama wa Maji katika Mfumo wa Mabonde ya Mto iliandaliwa kwa pamoja na Taasisi ya Jiografia na Uchunguzi wa Maji ya Nanjing (NIGLAS), Kituo cha Pamoja cha Utafiti cha China na Afrika, na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi ya nchini Tanzania (TAFIRI).

Akizungumza katika ufunguzi wa semina hiyo, katibu mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi nchini Tanzania, Riziki Shemdoe amesema, Ziwa Tanganyika, Ziwa Viktoria, na Ziwa Nyasa ni hifadhi muhimu ya maji duniani, na hivyo inahitajika juhudi za pamoja katika kuyalinda.

Naye Mwakilishi wa Balozi wa China nchini Tanzania Bw. Suo Peng amesema, nchi hizo mbili zimetekeleza awamu mbalimbali za ushirikiano katika utafiti wa usimamizi wa mazingira na maji na ulinzi wa rasilimali katika kanda ya Maziwa Makuu ya Afrika Mashariki tangu mwaka 2008, na matokeo ya tafiti hizo yametambuliwa na serikali na mashirika ya kimataifa.