Shirika la Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) linatekeleza mradi unaolenga kulinda vyanzo vya maji kwa watu milioni 11 wa mikoa ya Morogoro na Dar es Salaam Tanzania.
Happiness Minja, Afisa mradi wa WWF Tanzania unaojihusisha na uwekezaji endelevu katika Afrika, amesema chini ya mradi huu, WWF Tanzania itasambaza bila malipo miche ya miti 20,000 kwa watu ili wapande kwenye maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji vya Milima ya Uluguru mkoani Morogoro, ambavyo vinasambaza maji katika mikoa ya Morogoro na Dar es Salaam. Amefafanua kuwa miti mingi itakuwa ni matunda na viungo kama vile karafuu ambayo inasaidia sana kuhifadhi vyanzo vya maji.
Afisa kilimo wa mkoa wa Morogoro, Chesco Lwaduka amesema zaidi ya miche ya miti milioni 20 inahitajika kulinda vyanzo vya maji kwenye Milima Uluguru.