Viongozi wa Afrika Mashariki wametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano yanayoendelea nchini Sudan ambayo yamesababisha vifo vya takriban watu 56 na kujeruhi wengine karibu 600.
Ofisi ya Rais wa Kenya imesema kuwa viongozi wa Shirika la Maendeleo ya Serikali za Nchi za Afrika Mashariki (IGAD) wamefanya kikao cha dharura cha mtandaoni siku ya Jumapili ambapo walitoa wito huo.
Waliokuwa katika kikao hicho cha dharura ni Rais William Ruto wa Kenya, Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Ismail Omar Guelleh wa Djibouti, na Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.
Rais Ruto aliwaomba viongozi wa IGAD kuwa na msimamo thabiti kuhusu mzozo huo ili kurejesha amani nchini humo.
Viongozi hao waliazimia kuwatuma marais Kiir, Ruto na Guelleh haraka iwezekanavyo ili kupatanisha makundi yanayozozana. Viongozi hao pia wamezitaka pande mbili zinazohusika katika mzozo wa Sudan kutoa njia salama kwa ajili ya misaada ya kibinadamu katika mji wa Khartoum na mingine iliyoathiriwa.