Maelfu ya watu wameshiriki kwenye mbio za marathon zilizofanyika jana Jumapili huko Kampala, Uganda, zikilenga kukuza uelewa wa VVU na UKIMWI wakati nchi ikitarajia kumaliza janga hilo mwaka 2030.
Mbio hizo za marathon zinazojulikana kama “Mbio za Siku ya Kuzaliwa ya Kabaka” ambazo zimepewa kauli mbiu ya “Pambana Kumaliza VVU na UKIMWI hadi kufikia mwaka 2030”, zimefadhiliwa na serikali, makampuni, viongozi wa sekta ya utamaduni na watu mbalimbali kutoka tasnia ya burudani.
Katika salamu zake, Mfalme Ronald Muwenda Mutebi wa Buganda maarufu kama Kabaka, amesema mapambano dhidi ya ukimwi ni muhimu sana, na kusisitiza kwamba wanataka watu wawe hai na kuwaangalia ndugu zao wenye ugonjwa huo.
Naye msemaji wa Wizara ya Afya Emmanuel Ainebyoona amesema Uganda hadi sasa imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya VVU lakini marathon hiyo ni muhimu katika kukuza uelewa.