Jumuiya ya Nchi za Kiarabu yafanya mkutano wa dharura juu ya mapambano ya kijeshi nchini Sudan
2023-04-17 09:23:53| CRI

Jumuiya ya nchi za Kiarabu (AL) imefanya mkutano wa dharura mjini Cairo, ambapo wajumbe wa nchi za kiarabu walijadiliana mapambano ya kijeshi yanayoendelea nchini Sudan.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo, baraza la AL la ngazi ya wajumbe wa kudumu lilisisitiza ulazima wa kusimamisha mara moja mapambano yote ya silaha kwa ajili ya kulinda raia na ukamilifu wa ardhi na mamlaka ya Sudan.

Wajumbe wa nchi za kiarabu walihimiza pande zote za Sudan zirudie tena kwenye njia ya amani katika kutatua migogoro, na kuonya hatari ya kuongezeka kwa vurugu.

Wakati huohuo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Bibi Cindy McCain jana alisema, shirika hilo litasitisha kwa muda shughuli za kibinadamu nchini Sudan, siku moja baada ya wafanyakazi wake watatu kuuawa katika wilaya ya Kabkabiya jimboni Darfur Kaskazini nchini humo.