Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji na usafishaji madini
2023-04-18 18:54:14| cri

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameshuhudia kusainiwa kwa mikataba ya makubaliano kati ya Serikali na Kampuni tatu za madini kutoka Perth nchini Australia, ambapo amesema tani milioni 18.5 zenye asilimia 4.5 ya madini adimu yamegundulika katika Kijiji cha Ngwala, Songwe, na yatachimbwa kwa zaidi ya miaka 20.

Akizungumza jana baada ya kushuhudia kusainiwa kwa mikataba hiyo, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, Rais Samia amesema yapo maeneo ambayo zamani yaliaminika ni masikini yasiyo na rutuba na yasiyo na vyanzo vingine vya fedha, lakini yana utajiri mkubwa chini ya ardhi. Amesema mikoa ya Lindi na Morogoro ipo katika ukanda wa madini Kinywe, na Mkoa wa Songwe upo katika ukanda wenye madini adimu, na hiyo ndio sababu miradi hiyo ipo Chilalo mkoa wa Lindi, Epanko wilayani Ulanga, na Ngwala wilayani Songwe.