UNHCR na EAC zashirikiana tena katika kutatua suala la wakimbizi la kikanda
2023-04-18 09:11:32| CRI

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimesaini kumbukumbu ya maelewano  kwa ajili ya kurejesha na kuimarisha ushirikiano katika kutatua suala la wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi ambao wanahitaji ulinzi wa kimataifa kwenye kanda hiyo.

Taarifa iliyotolewa na EAC imesema, kumbukumbu hiyo ilisainiwa na katibu mkuu wa EAC Peter Mathuki na mkurugenzi wa kikanda wa UNHCR anayeshughulikia masuala ya maeneo ya Mashariki, Pembe ya Afrika na Maziwa Makuu Clementine Nkweta-Salami mjini Arusha, Tanzania. Ushirikiano huo unalenga kuunga mkono nchi wanachama wa EAC kuweka mazingira mazuri katika kutatua suala la wakimbizi, ikiwa ni pamoja na kurejea nyumbani kwa hiari na kuendelea kujiunga na jamii.

Mathuki alisisitiza tena kuwa EAC inadhamiria kuhimiza mpango wa utatuzi wa suala la kikanda la wakimbizi. Naye Nkweta-Salami alisema UNHCR itashirkiana na EAC katika kuhimiza na kulinda haki za binadamu za wakimbizi wa Afrika Mashariki.