Serikali ya Tanzania imejipanga katika kuhakikisha inakuwa na miundombinu bora ya mawasiliano yenye kutumia teknolojia ya kisasa itakayoleta tija na ufanisi katika kuongeza uzalishaji na ujenzi wa uchumi pamoja na kuimarisha usalama na ulinzi wa Taifa.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Nape Nnauye, jijini Dodoma, katika hafla ya utiaji saini kati ya Kampuni ya Mawasiliano ya Simu ya Tanzania (TTCL) na Kampuni ya HUAWEI ya China kuhusu upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Wilaya 23. Amesema serikali itahakikisha Mkongo huo wa Taifa unafika katika ngazi ya mkoa, wilaya na katika mipaka ya nchi, na kwamba tayari mikoa yote nchini humo imeunganishwa katika Mkongo wa Taifa ambao umefika katika vituo vya mipakani vimepakana na nchi jirani.