Kenya yapanga kuwaondoa raia wake 3,000 nchini Sudan kutokana na mapigano yanayoendelea
2023-04-18 09:10:56| CRI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Diaspora wa Kenya Bi. Roseline Njogu ametangaza mipango ya kuwaondoa raia wake 3,000 nchini Sudan kutokana na mapigano ya kijeshi.

Ameongeza kuwa ingawa anga ya Sudan imefungwa, nchi hiyo imeunda timu ya kiufundi ya mashirika mbalimbali ambayo inafuatilia hali inavyoendelea kwa wakati huu.

Bi. Njogu amesema kuwa wanakusanya vifaa vyote vinavyohitajika ili kuwaondoa raia wa Kenya mara tu anga ya Sudan itakapokuwa wazi na utakapokuwepo uwezekano wa kuwahamisha watu kwa usalama.

Amesema Kenya imedhamiria kuhakikisha raia wake wote wanaokolewa salama na kurudishwa nyumbani kama maisha yao yakiwa hatarini au katika janga la kibinadamu.

Pia alitoa wito kwa pande zinazopigana kuwa na amani na kufanya mazungumzo ili kutatua tofauti zao.