Watanzania 29 washinda shindano la ujuzi wa kufundisha lililoandaliwa na taasisi za kitaaluma za Tanzania na China
2023-04-18 09:27:39| CRI

Wanafunzi 29 kati ya 105 wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Tanzania Jumatatu walitunukiwa tuzo baada ya kushinda shindano la kwanza la ujuzi wa kufundisha.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa kwa pamoja na Kitivo cha Ualimu (SoED) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Kituo cha Pamoja cha Utafiti wa Elimu cha China na Afrika (SA-JoCER), yalilenga kuwawezesha walimu wanafunzi kuonesha ujuzi, umahiri na ubunifu wao.

Madaha Ndaki, mwanafunzi wa mwaka wa tatu anayesomea shahada ya kwanza ya sanaa katika elimu, alisema amefurahi kushinda kwenye kitengo cha stadi za kufundisha lugha ya Kichina, na ushindi huo umempa motisha ya kuwa na uwezo wa kuwafundisha Watanzania lugha ya Kichina baada ya kumaliza masomo yake, kwani lugha ya Kichina ni chachu ya kufungua milango ya ajira kwa makampuni ya Kichina yanayofanya kazi nchini Tanzania.

Mashindano hayo yalishirikisha masomo 10 tofauti yaliyochaguliwa katika mihtasari ya shule za sekondari, yakiwemo masomo ya biolojia, kemia, fizikia, hisabati, uraia, historia, jiografia, Kiswahili, Kiingereza na masomo ya lugha ya Kichina.