Kenya inaazimia kuvutia wawekezaji wa China kuanzisha viwanda vya utengenezaji bidhaa katika maeneo yake maalum ya kiuchumi ili kukuza mauzo ya nje ya nchi hiyo.
Akiongea na Shirika la habari la China, Xinhua, mjini Nairobi Kenneth Chelule, Kaimu Afisa mkuu Mtendaji wa Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya Kenya, alisema nchi hiyo inalenga wawekezaji wa China katika sekta za umeme, nguo, dawa na vifaa tiba, pamoja na sekta ya lifti na ngazi za umeme.
Alibainisha kuwa Kenya imedhamiria kutegemea teknolojia ya kisasa kutoka kwa wanaviwanda wa China ili kutengeneza bidhaa zenye ushindani kimataifa. Chelule aliongeza kuwa Kenya imesaini mikataba kadhaa ya kibiashara na mashirika makubwa ya kibiashara na nchi kama vile za Umoja wa Ulaya, Uingereza na Marekani, kutoa masoko ya faida kwa bidhaa zinazotengenezwa nchini humo.
Anatumai kuwa watengenezaji wa bidhaa kutoka China pia wataisaidia Kenya kubadilisha bidhaa zake za nje na kuisaidia kuondokana na bidhaa za kilimo.