Waislamu wa China na duniani kote hivi sasa wapo kwenye shamra shamra za sikukuu ya Eid al-Fitr wakisherehekea baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Hapa nchini China baada ya kumaliza sala ya Eid inayofanyika asubuhi na mapema, Waislamu wa makabila madogomadogo wanacheza dansi ili kusherehekea katika maeneo ya umma. Muziki huo wa furaha na dansi unawavutia watalii wengi, ambao huwa wanajiunga na sherehe hizo.
Wakati huohuo wanawake wengi wa Waislamu wa China wanakwenda kwenye vibanda vya sokoni na supermarket kununua chakula kwaajili ya sherehe ya sikukuu ya Eid. China ikiwa na Waislamu wapatao milioni 20, mbali na Beijing sikukuu hii pia inasherehekewa katika mikoa mingine, kama vile Qinghai, Gansu na Ningxia. Na katika mji wa kusini mwa China wa Guangzhou, Waislamu pia walikusanyika katika Msikiti wa Saad Bin Abi Waqqas katika eneo la katikati mwa jiji kufanya ibada ya sala ya Eid.
Na katika Mkoa wa Gansu kaskazini magharibi mwa China, karibu Waislamu milioni 1.8 wa makabila mbalimbali walisherehekea Eid al-Fitr jana. Saa mbili asubuhi, karibu Waislamu 800 walihudhuria ibada katika Msikiti wa Nanguan huko Lanzhou, mji mkuu wa jimbo hilo. Hivyo leo katika kipindi cha Ukumbi wa Wanawake tutaangalia wanawake na sikukuu ya Eid al-Fitr hapa nchini China.